Nani Mchezaji bora wa Msimu 2015-16 Ligi Kuu?


Ligi Kuu Bara imeisha Yanga wakitwaa Ubingwa Azam FC na Simba zikishika nafasi ya pili na ya tatu, Nani anastahili kuwa mchezaji bora wa msimu?
POLL
Kampeni za 2015-16 Ligi Kuu zikiwa zimemalizika, ni wakati sasa wa kuamua nani anastahili kuwa mchezaji bora wa msimu.

Ni mchezaji gani anastahili kupata tuzo ya mchezaji bora?

Donald Ngoma, Thabani Kamusoko, Shomari Kapombe, Farid Mussa, Juma Abdul na Amissi Tambwe hali kadhalika na Aishi Manula wakiwa wameng'ara na mmoja kati yao anastahili kuwa mshindi.

DONALD NGOMA

Mzimbabwe huyu alianza msimu kwa kasi, amewashinda nguvu, kasi na maarifa mabeki wengi wa VPL msimu huu. Akicheza na Tambwe katika safu ya mashambulizi ya Yanga, Ngoma amefunga magoli 17 hadi sasa huku akisaidia magoli zaidi ya kumi.
Amesabisha mikwaju mingi ya penalti kwa timu pinzani, pia walinzi wengi wamelambwa kadi nyekundu katika harakati za kumdhibiti mshambulizi huyo mwenye kukimbia kikakamavu.
THABAN KAMUSOKO

Mchezaji bora wa msimu? Inawezekana pia. Mzimbabwe huyo anakumbukwa kwa goli lake la dakika ya mwisho wakati Yanga ilipoifunga 1-0 African Sports katika game ya mzunguko wa kwanza. Amekuwa akitandaza pasi, kukaba kwa nguvu, kusaidia kutengeneza magoli na magoli yake 6 katika msimu wake wa kwanza yanamfanya kuonekana bora zaidi.
FARID MUSSA

Winga hatari kabisa ambaye kiwango alichokionyesha msimu huu hakina mpinzani na kinamfanya kuingia kwenye kikosi bora cha msimu huu pasipo kupigwa kutokana na mchango alioutoa kwa timu yake ya Azam lakini pia timu ya taifa.
Mussa analazimika kumshukuru kocha Stewart Hall wa Azam ambaye alichangia kupandisha kiwango chake na hivi karibuni mchezaji huyo huenda akajiunga na timu ya Tenerife Deportivo inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Hispania baada ya kufuzu majaribio aliyofanya kwa wiki tatu .
AMISSI TAMBWE

Idadi ya mabao 21 aliyoifungia Yanga msimu huu ni wazi anastaili kuwa kwenye kikos cha wachezaji 11 bora waliofanya vizuri msimu huu uliomalizika siku za karibuni.
Tambwe amekuwa akipondwa kuwa ni mchezaji wa kawaida lakini amekuwa na madhara makubwa anapokuwa kwenye lango la timu pinzani uwezo wake wa kufunga kwa kutumia kichwa na miguu umemfanya kuibuka mfungaji bora kwa mara ya pili akiwa na timu za Simba na Yanga.
JUMA ABDUL

Beki wa Yanga anayetajwa kuwa mchezaji bora msimu huu kutokana na mchango wake kwenye kikosi cha Yanga na hata timu ya taifa, mabao mengi yaliyofungwa na Amissi Tambwe na Donald Ngoma yametokana na krosi za Juma ambazo mara zote zimekuwa na matunda kutokana na utaalamu aliokuwa nao.
AISHI MANULA

Manula ndiye kipa aliyeidakia Azam mechi nyingi za ligi ya Vodacom kuliko msaidizi wake Mwadini Ali, lakini pia kipa huyo aliipa ubingwa wa Kombe la Kagame timu hiyo bila kufungwa hata bao moja na pia alifanya kazi kubwa ya kuokoa hatari nyingi kwenye lango la Azam ilipocheza na Esperance ya Tunisia kwenye michauano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
IBRAHIM AJIB

Kiungo mshambuliaji wa Simba ambaye akuwa mchezaji muhimu kikosi cha kwanza cha Jackson Mayanja licha ya kutocheza mechi za mwisho za kukunja jamvi la Ligi Kuu Bara, mchango wake upo dhahiri kwani ameweza kuwafungia Wekundu wa Msimbazi magoli 9. Umahiri wake dimbani na ari ya kutaka kufanya vizuri zaidi ni moja ya mambo yanayompa fursa ya kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania mchezaji bora wa msimu wa Goal.
SHOMARI KAPOMBE

Ukiwa msimu wake wa pili Azam FC, Shomari Kapombe amekuwa chachu ya mafanikio ya Azam kwa kutimiza majukumu yake kama beki na kuifungia timu yake mabao 8 ambayo hakuna beki aliyeweza kufikia rekodi yake msimu huuu.
JEREMIAH JUMA

Mshambuliaji wa Tanzania Prison, ana uwezo mkubwa dimbani na mchezaji asiyefanya makosa anapokabili lango la wapinzani, ni Mtanzania pekee mwenye magoli mengi katika Ligi Kuu Bara msimu ulioisha akiwa ametikisa kamba mara 11; Amejizolea umaarufu kwa kuzifunga Yanga, Azam na Simba.
SHIZA KICHUYA

Winga wa Mtibwa Sugar, amefanya kazi nzuri chini ya kocha Mecky Maxime. Na saini yake inawaniwa na klabu kubwa za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Yanga na Simba. Maxime anajivunia kukuza kipaji cha nyota huyu, kazi inabaki kwako shabiki kuamua kama anastahili kuwa mchezaji bora wa msimu uliopita!

Previous
Next Post »